Historia

Wamisionari wa kwanza wa Kanisa la Moravian walikuja Tanzania mwishoni mwa karne ya 19. Kituo cha kwanza cha Moravian Misheni kilianzishwa Rungwe Kusini mwa Tanzania mwaka 1891. Kituo kingine cha Magharibi mwa Tanzania kilikabidhiwa kwa Bodi ya Moravian huko Herrnhut, Ujerumani, na ‘London Missionary Society’ mwaka 1897. Kutokana na juhudi kubwa ya uinjilishaji, hivi vituo viwili vyenye ukaribu vilikua na vikawa makanisa makubwa yaliyoenea maeneo mbali mbali katika sehemu za kusini na magharibi mwa Tanzania. Kila kimoja kina jimbo lake. Ushirikiano kati ya vituo hivyo ulikuwepo tangu mwanzo wa kuanzishwa kwao. Wamisionari waanzilishi walikuwa wameanzisha mawasiliano mwanzoni mwa mwaka 1899. Baadaye walianza kukutana na kubadilishana uzoefu na hivyo, haya majimbo mawili yalianzisha ushirikiano wa mambo mbalimbali. Mwaka 1965 walikubaliana kuanzisha bodi ya pamoja ya kujadili na kukubaliana juu ya masuala yanayoendana katika majimbo hayo. Mwaka 1968 haya majimbo mawili yaliamua kuanzisha Chuo cha Theolojia cha Moravian kama washarika kwa kutoa mafunzo ya wahudumu. Mwaka 1976 jimbo la kusini liligawanywa katika majimbo mawili tofauti, Jimbo la Kusini na Jimbo la Kusini-Magharibi.

Pamoja na kuundwa kwa majimbo mapya haja ya kuanzisha Kanisa la Moravian nchini Tanzania kama bodi ya Kitaifa ya kuratibu na kuunganisha kazi ikawa kubwa zaidi. MCT kama kanisa linaendesha na kusimamia ubia, mipango na kuyawakilisha majimbo ndani na nje ya nchi. Tarehe 4 Agosti 1986, wajumbe kutoka majimbo manne ya Moravian walikutana Sikonge na kuazimia kuanzisha rasmi MCT kama kanisa ili kuwaunganisha Wamoravian wote Tanzania. Tarehe 23 Novemba 1986 MCT lilizinduliwa rasmi na mwezi Aprili, 1987 lilisajiliwa na serikali. MCT lilitambuliwa rasmi na Sinodi ya umoja ya Unitas Fratrum katika mkutano wake huko Antigua, West Indies mwaka 1988. Leo, Kanisa la Moravian Tanzania lina majimbo 7 yanayojitegemea lakini yanashirikiana, na jimbo la Kusini ni mojawapo.


Kiswahili